Thursday, August 4, 2011

Poulsen: Ulimwengu tafuta timu

KOCHA mkuu wa timu ya taifa ' Taifa Stars', Jan Poulsen amesema hana mpango wa kumuita mshambuliaji wa timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 23, Thomas Ulimwengu katika kikosi chake kwa sababu hana klabu.



Poulsen ametoa kauli hiyo katika kipindi ambacho taifa Stars inahitaji washambuliaji mahili kama alivyo Ulimwengu na Mbwana Samatta anayecheza katika klabu ya TP Mazembe ya DR Congo.

Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam, Poulsen alisema mchezaji huyo yuko katika kiwango kizuri na anastahili kuchezea timu ya taifa, lakini  anavyokosa timu ya kuchezea ndiyo inayomnyima nafasi katika kikosi cha Stars.

"Thomas ni mchezaji mzuri na alionyesha kiwango kikubwa sana katika mechi mbili alizocheza jijini Arusha dhidi ya timu ya taifa ya Shelisheli na anastahili kuchezea timu ya taifa, lakini tatizo lake ni moja tu! hana timu,”alisema Poulsen.

Alisema,"Binafsi nimeshazungumza na Ulimwengu na nikamshauri kuwa hivi sasa anapaswa kutafuta timu ili aweze kuchaguliwa  timu ya taifa kwa sababu ana kiwango kizuri ingawa amekaa muda mrefu bila kucheza hivyo anakosa vitu vichache ambavyo vinaweza kuigharimu timu ya taifa kwa hivi sasa endapo atapewa nafasi."

"Na atakapopata nafasi ya kucheza timu ya taifa ndipo atakapopata pia nafasi katika timu zingine kubwa za nje kama alivyofanya Mbwana Samatta kwa sababu mchezaji mwenye kiwango kizuri kama Ulimwengu ama kama alivyokuwa Samatta anapocheza timu ya taifa hawezi kukosa timu nje ya nchi”.

Kocha huyo alitoa maelezo hayo baada ya kuulizwa juu ya  mikakati yake ya kuwatumia vijana katika kikosi kitachocheza na Algeria katika mechi ya kuwania kufuzu mashindano ya Afrika (AFCON).

Akifafanua zaidi juu ya soka la vijana alisema,"timu ya vijana chini ya miaka 23 ina wachezaji  wazuri na wote wana uwezo mkubwa kwa sababu wamekaa pamoja ingawa sifa namba moja ya mchezaji kuitwa timu ya taifa ni mchezaji huyo kuwa na klabu inayoshiriki Ligi Kuu yoyote Duniani”:

Ingawa viwango vya vijana hao ni vizuri na baadhi yao hawataweza kuendelea kuichezea timu hiyo kwa sababu ya umri wao hivyo wanapaswa kuchangamkia nafasi ya kupata timu za Ligi Kuu haraka ili waingie Taifa Stars.

Wakati Poulsen akimshambulia mshambuliaji huyo na wenzake kutafuta timu hasa ndani ya nchi, Ulimwengu kwa upande wake amesema hawezi kucheza soka la Tanzania kwa ajili ya kuingia timu ya taifa.

"Anachosema kocha ni kweli na pia ni sahihi kabisa, lakini mimi siwezi kucheza soka la Tanzania kwa ajili ya kuingia timu ya taifa, mimi nina mikakati yangu ninayoisubiri na wakati utakapofika nitaiweka wazi kwa watanzania wote,"alisema Ulimwengu.

Alisema anatambua umuhimu wa timu ya taifa, lakini pili anazingatia maisha yake ya baadaye ya soka na kwamba hiki ndicho kipindi chake cha kuandaa maisha yake ya baadaye ambayo pia yanaweza kuisaidia Taifa Stars kwa siku za usoni kuliko hivi sasa.
                                                         Zoom for better video.
Thomas Ulimwengu ni miongoni ya wachezaji mahili waliyowahi kuichezea timu ya FC KILIMANJARO ya SWEDEN.

No comments:

Post a Comment